HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Kagasheki awashukia vigogo Hifadhi Ngorongoro

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki ametangaza kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliokwamisha mradi wa kuwasaidia wafugaji wa hifadhi hiyo ulioahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2008.

Akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro na viongozi wa NCAA mara baada ya kuelezwa kuhusu kukwama kwa mradi huo, Balozi Kagasheki alisema lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya viongozi hao.

“Haiwezekani mradi ulioahidiwa mwaka 2008 leo hii ukwame, waliohusika kuukwamisha ni lazima wakae pembeni. Ninakwenda Dar es Salaam ila wakae wakijua kuwa barua zao zinakuja” alisema Kagasheki na kuongeza;
“Kabla sijaondolewa wizarani kutokana na matatizo kama haya, mtaondoka ninyi kwanza.…, kukwama kwa mradi huu kutawafanya wananchi wamchukie Rais Kikwete na wanasiasa,” alisema Balozi Kagasheki.

Awali, Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro, Bruno Kawasange alisema mradi huo, ambao ulifikia hatua nzuri, umesitishwa na PPRA kwa maelezo kuwa taratibu hazikufuatwa katika kumtafuta mtaalamu mwelekezi.

Kawasange alisema awali, mtaalamu mwelekezi wa mradi huo, alipatikana nchini Ufaransa na tayari taratibu kadhaa zilianza ikiwa ni pamoja na kutolewa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa.
Hata hivyo, alisema katika hatua za mwisho, PPRA iliwataka kuanza upya taratibu za kumpata mtaalamu huyo, kwa maelezo kwamba taratibu za kisheria hazikufuatwa.

Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, Justice Muumba alisema licha ya kutakiwa kuanza upya kwa taratibu za kumpata mtaalamu mwelekezi, mambo mengi ya msingi yalikuwa yamefikiwa.

Katika mradi huo, NCAA kwa kushirikiana na Baraza la Wafugaji, walikuwa waanzishe mradi mkubwa wa ufugaji wa kisasa na kiwanda cha kusindika nyama na maziwa ambacho kingesaidia kumaliza matatizo ya wakazi wa Ngorongoro hasa ya njaa.

Apokewa kwa mabango
Katika ziara yake hiyo, Waziri Kagasheki alipokewa kwa mabango na wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro, yaliyokuwa yakieleza jinsi wanavyoshindwa kufanya shughuli za kilimo kutokana na kubanwa na NCAA.

Waziri Kagasheki, ambaye alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o ole Telele na maofisa kadhaa wa Serikali, alikutana na mabango hayo alipofika katika Kijiji cha Mokilali Kata ya Ngorongoro.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: “Njaa inatuuwa Ngorongoro,” “Tunalaani kauli ya Mkuu wa Mkoa Arusha kuwa Ngorongoro hakuna njaa,” “Tumechoka kuwa watumwa, tunataka uwiano Ngorongoro.”
Katika mkutano huo, wananchi karibu wote, waliopewa nafasi ya kuzungumza walieleza tatizo kubwa la njaa ambalo linawakabili wakisema linasababisha watoto kufariki, kuugua magonjwa ya utapiamlo, wanaume kutelekeza familia zao na vijana kukimbilia mijini kufanya kazi za ulinzi.

Diwani wa Kata ya Enduleni, James Moringe alisema karibu kila kaya katika tarafa hiyo, sasa inakabiliwa na njaa kali na wananchi hawana chakula kutokana na kuzuiwa kwa shughuli za kilimo cha bustani bila kuwapo kwa utaratibu mwingine wa kuwapatia chakula.

“Kwanza tunakanusha taarifa ya Mkuu wa Mkoa wetu, Magesa Mulongo kuwa Ngorongoro hakuna njaa, sisi tunamshangaa sana mkuu wa mkoa na tunalaani kauli yake,” alisema Moringe
 Moringe ambaye pia ni Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Wilaya ya Ngorongoro na Katibu wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, alisema kauli ya mkuu wa mkoa ni ya kulaaniwa kwa kuwa inakidhoofisha chama hicho.

“Kauli za viongozi kama huyu hazina masilahi kwa chama chetu, leo hii ukipita Arusha mjini na nguo za kijani unazomewa kutokana na kauli kama hizi, watu wana njaa wewe unasema hakuna njaa,” alisema Moringe.

Katibu wa Mbunge wa Ngorongoro, William Ole Seki na Diwani wa Viti Maalumu (CCM), Agnes Sandai, walisema tatizo na njaa kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro limekuwa sugu sasa na hakuna taratibu zozote za kuwapa njia mbadala wananchi baada ya kuwazuia kulima ndani ya hifadhi.
Seki alisema kwa sasa wakazi wa tarafa hiyo hawajitambui kama ni raia wa Tanzania au la kwa kuwa wanaishi maisha ya shida wakati Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inapokea mabilioni ya fedha kutokana na uhifadhi wa wanyama.
Kwa upande wake, Sandai alisema lengo la kuanzishwa Ngorongoro lilikuwa ni kusaidia uhifadhi, kuongeza utalii na kuwaendeleza wenyeji wa Ngorongoro lakini kinachofanyika sasa ni tofauti kwani wenyeji wametelekezwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Ole Telele alisema walimwomba waziri afike mwenyewe Ngorongoro ili kujionea tatizo la njaa.

Kwa upande wake, Lembeli alisema kamati yake ilitembelea vijiji kadhaa na kujiridhisha kuwa kuna haja ya kutafutwa ufumbuzi wa haraka wa kuwapatia chakula wakazi wa Ngorongoro. Kawasange alikiri kuwapo kwa tatizo la njaa na alisema tayari NCAA ilitenga kiasi cha Sh315 milioni kununua tani 900 za chakula.
“Tatizo ambalo lilijitokeza ni kuchelewa kupata kibali, lakini pia tumeweza kununua chakula kingine cha dharura magunia 2,000 ambayo tayari tuliyagawa. Bado tunaendelea kununua mahindi lakini tunakwaza na utaratibu wa ununuzi wa kutangaza tenda kwanza,” alisema Kawasange.

Akizungumza suala hilo la njaa, Waziri Kagasheki aliiagiza Mamlaka ya Hifadhi kuhakikisha inanunua chakula chote kinachohitajika na kukigawa kwa wananchi na kama kuna matatizo ya vibali vya kukinunua katika ghala la taifa na masuala mengine, wawasiliane na wizara haraka iwezekanavyo.

“Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro (Kawasange), maelezo yako hayajaniridhisha kwani kama mlipata matatizo katika kununua mahindi Ghala la Taifa mngetujulisha mapema, hamuwezi kusubiri mambo ya tenda watu wanakufa njaa,” alisema Waziri Kagasheki.

Kuhusu maombi ya wananchi hao ya kilimo cha kujikimu, waziri Kagasheki alisema ataunda timu huru ya wataalamu kufanya uchunguzi juu ya ombi hilo na kuona kama kuna uwezekano wa kupatikana maeneo ya kilimo ndani ya hifadhi hiyo.
 
MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: