Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi
ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza
1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia
darasa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban
miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba
katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu
Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba
kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa
Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya
sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka
1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti
hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama
za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo
yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha
vyeti vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa
mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka
ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge,
tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu
walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu,
wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu
waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa,
maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati
tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu
kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea
ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu
Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi
ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena
jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi
ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili
kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni
marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa
akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya
Sekondari ya Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu
katika shule hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo
(jina tunalihifadhi kwa sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu wa
kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster)
wakati hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa
shule baada ya aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni
wafanyabiashara kwa hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana
walimpandisha tu madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki
yake huyo na kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama
ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu
angechukuliwa hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na
kujipa cheo cha umeneja wa shule.”
Suala la uwezo na elimu ya Mulugo liliibua mjadala
siku chache zilizopita baada ya kutoa kauli nchini Afrika Kusini
aliponukuliwa akisema Tanzania ni muungano wa nchi mbili ambazo ni
Tanganyika na Zimbabwe badala ya Zanzibar.
Alikotokea
Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika kijiji
alichozaliwa cha Udinde, Kata ya Kapalala wilayani Chunya mkoani Mbeya
na alisoma Shule ya Msingi ya Rukwa.
Mmoja wa walimu waliomfundisha aliyejitambulisha
kwa jina la Nyoni anasema anakumbuka kwamba Naibu Waziri huyo 1989 na
wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Hamimu Hassan.
“Mimi nilihamia hapa 1989 nikitokea Shule ya
Msingi Kapalala. Kulikuwa na mwalimu mmoja tu kwa hiyo nikawa wa pili.
Namfahamu Mulugo wakati huo akiitwa Hamimu Hassan. Sijui kabla hapo
alikuwa akitumia jina gani,” alisema Nyoni anayetarajia kustaafu kazi ya
ualimu mwakani.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa Waziri Mulugo
anayeishi kijijini hapo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini
alikiri kuwa awali waziri huyo alikuwa akiitwa Philipo Augustino Mulugo.
“Philipo amesomea hapo Rukwa, ambayo ni Shule ya
Msingi na alikwenda Kijiji cha Mkulwe kabla ya kwenda Mbeya kuwa
Mwalimu. Sijui kama alirudia shule,” alisema ndugu huyo.
Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Peter Kayuti
alikiri kumfahamu Waziri Mulugo tangu enzi za utoto na kwamba alirudia
darasa la saba, lakini alisema hakumbuki jina la pili alilolitumia. “Ni
kweli Philipo alirudia shule, lakini sijui kama alitumia jina jingine
zaidi ya hilo la sasa,” alisema Kayuti.
Mwalimu aliyemfundisha katika Shule ya Sekondari Mbeya ambaye
pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alikiri kumfahamu kwa jina la Hamimu
Augustino, lakini akasema hafahamu lilibadilika lini.
“Ni kweli, nilimfundisha Waziri Mulugo na alikuwa
akiitwa Hamimu Agustino. Sidhani kama ni jambo geni kwa wanafunzi hasa
wa zamani kurudia shule… Zamani ilikuwa kawaida kwa kuwa shule zilikuwa
chache. Sijui alibadilisha jina hilo lini, lakini hilo ni suala la
kisheria tu,” alisema mwalimu huyo.
Utata wa majina
Mwalimu mwingine aliyewahi kufanya kazi na Waziri
Mulugo katika Shule ya Southern Highlands alisema waziri huyo alikuwa na
tabia ya kuchanganya majina yake ya awali ili kuficha cheti alichoombea
kazi.
“Yule alikuwa mjanja sana, ndiyo maana ukiangalia
kadi zake zilikuwa na majina mengi tu na yana badilika. Leo atasaini
barua kwa jina hili kesho lile. Mara utaona ameandika kifupisho cha
PHDA, yaani Philip Hamimu Dick Agustino, mara Mulungu EDM, mara Mulugu
D. Philip,” alisema mwalimu huyo na kuongeza:
“Amekuwa akijaribu kulibadilisha jina la Mulungu
kuwa Mulugu mwisho amelipeleka kuwa lake la awali la Mulugo. Yote hayo
ni kuficha tu ukweli kwamba alitumia cheti cha Dick Mulungu,” alisema
mwalimu huyo.
Mmoja wa wakuregenzi katika Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi (jina tunalihifadhi) alisema: “Ili mwalimu wa
sekondari awe headmaster (mkuu wa shule) ni lazima awe na shahada ya
kwanza kutoka kwenye chuo kikuu kinachotambulika. Anatakiwa pia kuwa na
uzoefu wa kazi wa miaka isiyopungua minane.”
Kuhusu kughushi vyeti mkurugenzi huyo alisema,
ikigundulika kuwa mwalimu ameghushi cheti anafukuzwa kazi mara moja,
lakini alikiri kwamba katika shule binafsi inawezekana walimu wasio na
sifa wakapenya, lakini wakaguzi wakibaini hutoa maelekezo wafukuzwe.
“Kwanza siku hizi ili mwalimu aajiriwe ni lazima
akabidhi vyeti vyake wizarani na hupelekwa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta) ili kuhakikiwa. Zamani ukaguzi haukuwa makini kwa hiyo
inawezekana kuna watu wasio na sifa walipenya,” alisema.
Kuhusu kurudia darasa la saba, alisema sheria
haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba na kwamba wale waliorudia
hutumia mbinu zao kufanya hivyo.
“Sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la
saba. Ni kweli wengi wamerudia sijui wanatumia mbinu gani, lakini
hairuhusiwi. Ukishafanya mtihani wa darasa la saba mara moja ndiyo
basi,” alisema mkurugenzi huyo.
Msemaji wa wizara hiyo, Mtandi Bunyanzu kwa kila
swali aliloulizwa alisema hana uhakika hivyo asingeweza kutoa jibu
lakini kwa suala la kughushi vyeti, alisema ni kosa la jinai siyo kwa
walimu tu bali kwa kila mtu atakayebainika.
“Kughushi vyeti ni kosa la jina siyo kwa walimu tu, hata waandishi wa habari,” aliongeza Bunyanzu.
Kwa upande wake, Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta) halikuwa tayari kutoa matokeo ya mitihani ya Mulugo na badala
yake msemaji wa baraza hilo John Nchimbi alisema matokeo hayo ni siri ya
mtahiniwa na hawezi kupewa mtu mwingine.
MWANANCHI



No comments:
Post a Comment