Polisi bado wanachunguza kilichosababisha kifo cha Berezovsky
Kilichosababisha kifo cha tajiri Boris Berezovsky, mwenye umri wa miaka 67, bado hakijajulikana.
Tajiri huyo alikuwa akisakwa mno nchini Urusi, na anafahamika kuwa mpinzani mkali wa Rais
Zamani
alikuwa na mamlaka na ushawishi sana katika bunge la Kremlin, lakini
yote hayo yalididimia mara tu alipoingia Bw Putin, na Berezovsky
alikimbilia Uingereza kuanza maisha ya uhamishoni mwaka 2000.
Awali idara ya polisi ya Thames Valley
ilitangaza kwamba ilikuwa katika hatua za kuchunguza kifo cha mwanamume
mmoja mwenye umri wa miaka 67, katika eneo la Ascot, Berkshire.
Mwaka uliopita, Bw Berezovsky alishindwa katika
kesi ambayo aliwasilisha madai ya kutaka kulipwa pauni bilioni tatu,
dhidi ya tajiri anayemiliki klabu ya soka ya Chelsea ya Uingereza, Roman
Abramovich.
Bw Berezovsky alidai alitishwa na Bw Abramovich,
kiasi cha kuuza hisa za kampuni kubwa ya mafuta nchini Urusi, Sibneft,
kwa kiwango kidogo mno cha fedha, ikilinganishwa na thamani halisi ya
hisa hizo.
Madai hayo yalikataliwa moja kwa moja na hakimu
wa masuala ya biashara mjini London, na ambaye alisema Bw Berezovsky si
shahidi wa kuaminika.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya kimataifa,
Richard Galpin, alisema watu mbalimbali walimueleza kwamba Bw Berezovsky
alisongwa na mawazo kufuatia kushindwa katika kesi hiyo, na kuandamwa
na matatizo mbalimbali ya kifedha.
Tajiri huyo mkuu inasemekana alipoteza kiasi kikubwa cha mali katika
miaka ya hivi karibuni, na akiwa katika hali ya kulipa gharama
mbalimbali za kesi nyingi alizoziwasilisha mahakamani.
Rais Putin hakutaka urafiki wa Berezovsky
Bw Berezovsky pia aliweza kujirundikia mali
katika miaka ya 1990, akiuza magari ya Mercedes na vile vile magari
mengineyo yaliyoundwa nchini Urusi.
Boris Berezovsky alikuwa kati ya kundi dogo la
matajiri wakuu wa Urusi, na ambao walifurahishwa na kuangamia kwa siasa
za kikomunisti, na wakitumia waliowafahamu katika madaraka ya juu kwa
misingi ya kujitajirisha haraka.
Huku mamilioni ya raia wa Urusi wakitumbukia katika umaskini,
Berezovsky aliingia katika biashara, na kuuza magari, na pia kununua
hisa katika kituo kikuu cha matangazo ya televisheni nchini Urusi.
Aliwekeza pia katika shirika la ndege la Aeroflot, na vile vile katika kampuni ya mafuta.
Vile vile wakati huo alikuwa ni rafiki mkuu wa
rais wakati huo, Boris Yeltsin, na uhusiano huo ukampa mamlaka mno
katika bunge la Urusi.
Lakini Vladimir Putin akawa ni rais tofauti
kabisa, akiwa kiongozi wa Kremlin ambaye hakutaka hata kidogo kuelezewa
namna ya kuiongoza Urusi.
Ndipo hapo Berezovsky alipopoteza ushawishi wake katika Kremlin, na kutoroka hadi mjini London.
BBC SWAHILI



No comments:
Post a Comment