HATUA ya vyombo vya habari kulivalia njuga suala la kutekwa,
kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom
Kibanda haiwafurahishi watendaji wa serikali.
Vyombo kadhaa vya habari yakiwemo magazeti, vimekuwa na habari, makala
na maoni mfululizo kuisukuma serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi
iwasake na kuwafikisha mahakamani wahusika wa tukio la Kibanda ambaye
pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006).
Katika habari hizo, vyombo hivyo vinaeleza kushangazwa na kitendo cha
Jeshi la Polisi kushughulikia matukio mepesi haraka na kwa kutumia nguvu
nyingi, huku sakata la Kibanda na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka uchunguzi wake ukidorora.
Msukumo huo wa vyombo vya habari kuvisakama vyombo vya dola na baadhi
ya vigogo serikali kuhusika na matukio hayo umepokelewa kwa mtazamo
hasi.
Habari za uhakika zinasema kuwa vigogo kadhaa wameanza kuhaha kupanga
mikakati ya kuvizima vyombo hivyo, hususani magazeti ya Tanzania Daima
na Mtanzania ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuandika sakata hilo.
Katika mkakati huo, tayari gazeti la Mtanzania limeandikiwa barua na
Msajili wa Magazeti ambapo Kaimu Mhariri wake anatakiwa kwenda kujieleza
Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu habari iliyochapishwa Machi 20, mwaka
huu.
Akithibitisha kupokea wito huo, Mhariri wa Mtanzania, Kulwa Karedia,
alisema barua hiyo ina kumb. Na. IR/RN/336/57 ya Machi 21 mwaka huu, na
imesainiwa na Jamal Zuberi kwa niaba ya Msajili wa Magazeti.
Alisema kuwa Kaimu Mhariri wao anajulishwa, “Madhumuni ya wito huo ni
kujadili habari iliyochapishwa na gazeti lako toleo Na.7262 yenye kichwa
cha Urais wa damu.”
Karedia alisema kuwa habari husika iliyoandikwa na Mtanzania ilielezea
kuwa sakata la kushambuliwa kwa Kibanda limeanza kuibua tetesi na
kutaka Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ahojiwe kutokana na kauli
yake.
Membe alihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV Julai mwaka jana,
katika kipindi cha Dakika 45 na kudai kuwa anao maadui 11 wakiwemo
waandishi wa habari wawili ambao atawatwanga kweupe.
Hatua ya kutaka Membe ahojiwe ni kutokana na Kibanda kuumizwa ikiwa ni
takribani miezi tisa tangu kauli hiyo itolewe bila kufafanua maadui
zake aliwakusudia akina nani.
Hata hivyo gazeti hili lilidokezwa kuwa baadhi ya vigogo waandamizi wa
serikali, CCM na maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa wamekuwa na vikao
vya kujadili namna ya kunyamazisha magazeti hayo.
Lengo la mkakati huo ni kuhamisha mjadala ili wananchi wahangaike na mambo mengine wasahau sakata la kuteswa kwa Kibanda.
Miongoni mwa wanaohaha katika suala hili ni waziri mmoja machachari
ambaye anatajwa kuusaka urais kwa nguvu akishirikiana na kigogo mwingine
wa CCM.
Inadaiwa kuwa kumekuwa na vikao vya mfululizo ambapo vya mara ya
mwisho vimefanyika juzi kwa siku mbili ofisini na nyumbani kwa waziri
huyo jijini Dar es Salaam kujadili mkakati wao.
Miongoni mwa walioshiriki vikao hivyo yumo pia kigogo mmoja wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Baadhi ya mambo waliyojadili ni kuyafungia baadhi ya magazeti, hasa
Tanzania Daima na Mtanzania, ambayo wamesema yanafuatilia na kuripoti
sana habari za masaibu yaliyompata Kibanda.
Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu walikubaliana kwamba ni rahisi kuanza na Mtanzania kwa sababu za kimkakati na kisiasa.
Kwa sababu zao za kimkakati walikubaliana kuanza na Mtanzania na
kuliacha Tanzania Daima ambalo linamilikiwa na kiongozi wa upinzani.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kujiridhisha kwamba mchakato wa
kuvishitaki vyombo hivyo unaweza kuchukua muda mrefu na kuibua masuala
mengine wasiyotaka jamii iyajue.
Vigogo hao walienda mbali zaidi wakimhusisha Ofisa Mkuu Mtendaji wa
New Habari (2006), Hussein Bashe wakidai amekuwa akitumia magazeti ya
Rai na Mtanzania kuelekeza yaandike masuala yanayochafua serikali,
waziri mmoja na kundi lake na makundi kadhaa ndani ya CCM.
Ingawa suala la uraia wa Bashe lilishamalizika kwa Idara ya Uhamiaji
kuuthibitisha, mipango ya kundi hili sasa imejielekeza katika kuibua
upya suala hilo kisiasa ndani ya chama kwa kumtumia kijana machachari na
bingwa wa propaganda ambaye ana wadhifa mkubwa ndani ya chama.
Taarifa zinasema suala hilo litaibuliwa ndani ya vikao vikuu vya chama
vijavyo ili CCM iendelee kusisitiza haitambui uraia wake na iweke
shinikizo afukuzwe uanachama.
Vile vile waliweka mkakati kuwa shinikizo hilo litapelekwa hadi kwa
mwajiri wa Bashe, Rostam Aziz ili amwondoe kwenye cheo hicho au amfukuze
kazi kwa sababu magazeti yake yamekuwa hayatimizi malengo asilia
yaliyomsukuma kuyanunua.
Bashe ashangaa
Alipotafutwa Bashe jana kueleza kama ana taarifa za mikakati ya kikao
hicho, alijibu kwa kifupi; “Sijazipata taarifa hizo ila nitazifanyia
kazi.”
Bashe alikiri kupokea barua ya Msajili wa Magazeti ikiwataka wafike
kujieleza Jumatatu mchana, lakini akaongeza; “Hilo suala la uraia wangu
kama kweli wanaendelea nalo watakuwa wanajisumbua bure.”
Nape ang’aka
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnuye, alipoulizwa kama anafahamu ama ameshiriki vikao hivyo vya
mikakati ya kuyanyamazisha magazeti hayo, aling’aka na kusema CCM hawana
matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania.
“Hicho kikao kinafanyikaje? Mimi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, huyo
waziri anashughulika na wizara yake halafu huyo mtu wa Maelezo ana idara
yake,” alisema.
Nape alidai hajawahi kuonana na waziri mtajwa kwa muda mrefu na kwamba
hata hajui kama amerudi nchini tangu walipokutana nchini Afrika Kusini
wiki kadhaa zilizopita.
“CCM kama chama hatuna matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania, hizo
ni fitina zenu mnataka kutengeneza, vyombo hivi tunashirikiana vizuri
hata niliwahi kutembelea ofisi zao baada ya kuteuliwa na hata kwenye
ziara zetu mikoani tunavichukua,” alisema.
Waziri tajwa na kigogo mmoja wa Maelezo hawakupokea simu zao kutoa
ufafanuzi hata walipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hawakujibu.
Sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Kibanda
linafananishwa na lile la Dk. Ulimboka kwani hadi sasa uchunguzi wa
kuwasaka waliohusika unafanyika kimzaha.
Tangu alipoumizwa Dk. Ulimboka Juni 26 mwaka jana, ni mtuhumiwa mmoja
pekee amefikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo ingawa
inaelezwa kuwa alikuwa amerukwa na akili akajipeleka kanisani na kudai
kuhusika.
Zikiwa sasa ni wiki tatu tangu kujeruhiwa kwa Kibanda, hakuna
mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa na vyombo vya dola kuhusiana na tukio
hilo, ingawa ndani ya wiki moja Jeshi la Polisi limekamata na
kumchunguza Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred
Lwakatare kisha kumfikisha mahakamani akidaiwa kujihusisha na ugaini kwa
kutumia usahidi wa video.
TANZANIA DAIMA



No comments:
Post a Comment