HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » CCM YAWAWASHIA MOTO KAGASHEKI, AMANI


Dodoma. Wakati Kamati Kuu ya CCM imeamua kuumaliza mgogoro wa madiwani wake wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa kutoa onyo kwa viongozi wake, ndani ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), hakujatulia kwani kuna mpango wa kumwondoa Katibu Mkuu wake, Martin Shigela.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya vikao vya Kamati Kuu zimesema kwamba viongozi kadhaa wa chama hicho akiwamo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani wameonywa kutokana na mgogoro wa muda mrefu katika wilaya hiyo.
Wengine waliotakiwa kupewa karipio ni pamoja na  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye na Katibu wake, Averin Mushi ambao walitarajiwa kuhojiwa jana usiku.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo vinavyofanyika Mjini Dodoma zilisema hata ule uamuzi wa kuwazuia Amani na Kagasheki kufanya siasa umeonekana unaweza kuleta athari kwao na kwa chama chenyewe, hivyo kuamua kutoa onyo na madiwani waliokuwa wamefukuzwa uanachama kuachwa kuendelea na nyadhifa zao. Vyanzo hivyo vya habari vilieleza kuwa suala hilo lilikuwa tayari limeamuliwa, isipokuwa ilikuwa ni lazima wahusika waitwe kufahamishwa uamuzi dhidi yao badala ya kusikia kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, hadi jana wakati tunakwenda mitamboni ni viongozi wawili tu, waliokuwa wamehojiwa na Kamati Kuu ambao ni Buhiye na Mushi kwa kuwa tayari walikuwapo Dodoma wakiwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Balozi Kagasheki na Amani licha ya kwamba walikuwa wamewasili hapa, suala lao liliahirishwa kutangazwa kuwasubiri Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Yussuf Ngaiza na Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Janeth Kayanda waliochelewa kufika mjini hapa baada ya gari lao kuharibika.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema uamuzi wa Kamati Kuu ungetolewa baada ya kumalizika kwa hatua ya kuwahoji viongozi hao jana.
Mgogoro wa Manispaa hiyo unatokana na miradi iliyopangwa na Meya Amani, ambayo inapingwa na baadhi ya madiwani wa CCM wa Manispaa akiwamo Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii.
Hali ya siasa mkoani humo ilichafuka zaidi baada ya  Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Kagera kuwafukuza madiwani wanane kwa kosa la kumpinga Meya huyo na kupanga kumng’oa madarakani.
Madiwani hao ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Ngaiza(Kashai).
Hata hivyo, uamuzi huo wa kuwafukuzwa ulisimamishwa na Sekretarieti ya CCM ambayo ilisema kuwa Kamati Kuu ndiyo iliyokuwa na madaraka ya kutoa uamuzi wa mwisho dhidi yao na kuwataka kuendelea na kazi wakisubiri hatima yao.
Katika hatua nyingine, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), ambacho kilikuwa kimalizike jana kimeongezewa siku moja zaidi na kitafungwa rasmi leo.
Nape alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuwapa nafasi wajumbe wake kuipitia Rasimu ya Katiba.
UVCCM kwawaka moto
Baraza Kuu la UVCCM linakutana mjini Dodoma wiki hii pamoja na mambo mengine ni kupitisha jina la Katibu Mkuu mpya wa umoja huo.
Uteuzi huo unafanywa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, Sadifa Juma Khamis, ambaye inaelezwa kuwa ameamua kumwondoa Martine Shigela.
Habari za ndani kutoka katika umoja huo, zinasema mbali na muda wa Shigela kumalizika, kumekuwapo na mgogoro ndani ya UVCCM, baina yake na Sadifa tangu alipochaguliwa mwaka jana.
Habari hizo zinasema majina matatu yamependekezwa kwa nafasi hiyo, akiwamo Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda anayepewa nafasi kubwa. Wengine wanaotajwa kupendekezwa na Mwenyekiti na kusubiri baraka za Baraza Kuu ni wakuu wa Wilaya wawili, Elibariki Kingu (Igunga) na Anthony Mtaka (Mvomero).
Kutokana na unyeti wa nafasi ya Katibu Mkuu wa UVCCM, jana makundi ya umoja wa vijana yalikuwa yameanza kujikusanya mjini hapa kujadili, huku baadhi yakichambua ama kwa kuafiki au kupinga majina hayo.
Kuna taarifa kuwa uamuzi uliochukuliwa ni mwendelezo wa mvutano wa makundi ya wagombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Sadifa alikataa kulizungumzia kwa undani akisema lisubiri vikao vimalizike.
“Kwanza vikao havijajadili jina la mtu anayefaa kuwa katibu mkuu, siwezi kulizungumzia. Subiri vikao vikimalizika nitakuwa tayari kuzungumza,” alisema Sadifa.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: