*Ni yule anayehusishwa Rwanda
HATIMAYE Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekiri kuwa ofisa wake mwenye cheo cha Luteni Kanali, Colestine Seromba, ametoroka na hajulikani alipo. Limesema Luteni Kanali Serombo alitoroka Desemba 18, mwaka jana, siku chache kabla ya kufikishwa kwenye mahakama ya kijeshi kujibu mashitaka yaliyokuwa yakimkabili ambayo hata hivyo hayakutajwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba, licha ya kukiri kutoweka kwa Luteni Kanali Serombo, alikana taarifa kwamba alitoweka na nyaraka nyeti za jeshi.
Taarifa hii ya JWTZ imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya gazeti hili, wiki iliyopita kuripoti kutoweka kwa Luteni Kanali Serombo.
Likinukuu vyanzo vyake vya habari vilivyoko ndani ya jeshi, MTANZANIA Jumapili, liliripoti kuwa ofisa huyo anayeaminika kuwa na asili ya Rwanda, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha, huku akiacha wingu la mashaka kwamba, hatua yake hiyo inaweza ikawa imeambatana na kupotea pia kwa baadhi ya taarifa muhimu za kijeshi.
Ni taarifa hizo ndizo zilizolilazimisha JWTZ jana kulitolea ufafanuzi suala hilo, ambapo pamoja na kuthibitisha kutoweka kwake, lilishindwa kueleza alikokimbilia na tuhuma zilizokuwa zikimkabili kabla ya kutoroka.
“Ofisa huyu alikuwa na tuhuma za makosa ya kijeshi na wakati mchakato wa kumfungulia mashitaka ukiwa unaendelea, alitoroka usiku wa tarehe 17 kuamkia 18 mwezi Desemba mwaka jana.
“Kijeshi kosa la utoro halifutiki, yaani halina ‘Time Bar’, kwa maana hiyo bado ofisa huyu ni mtoro kwa kipindi cha zaidi ya miezi minane,” alisisitiza Meja Komba.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Hata hivyo, taarifa hiyo ya Meja Komba kwa waandishi wa habari haikueleza mahali alipokimbilia wala haikugusia ripoti zinazoeleza kuwa amekimbilia nchini Rwanda, badala yake ilisema juhudi za kumsaka bado zinaendelea.
Meja Komba alisema Luteni Kanali Colestine Seromba ni Mtanzania, hana asili yoyote ya Rwanda, bali ni mzaliwa wa Kijiji cha Rukira, mkoani Kagera na aliyesoma Shule ya Msingi Rukira na baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Rulenge, kabla ya kusoma elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Minaki, jijini Dar es Salaam.
“Napenda kusema kwamba Luteni Kanali Colestine Seromba ni Mtanzania na hana asili yoyote ya Rwanda, ni mzaliwa wa Kijiji cha Rukira, mkoani Kagera na elimu yake alipata hapa nchini kuanzia Shule ya Msingi Rukira, Sekondari ya Rulenge na baadaye Minaki High School,” alisema Meja Komba.
Aidha, Meja Komba pia alitoa ufafanuzi kuhusu hofu ya Luteni Kanali Seromba kutoweka na nyaraka nyeti za jeshi kwa kueleza kuwa katika kipindi cha utumishi wake jeshini, ofisa huyo alikuwa ni mkufunzi wa masomo ya kompyuta (IT) katika Chuo cha Jeshi.
Alisema kulingana na wadhifa wake, alikuwa na uwezo wa kusoma baadhi ya nyaraka zilizomfikia ofisini kwake kwa ajili ya utekelezaji au kwa taarifa, lakini kabla hajatoroka alikabidhi vifaa vyote vya ofisi aliyokuwa akiisimamia kwa uongozi wa jeshi.
“Kulingana na cheo alichofikia na madaraka aliyokuwa nayo, alikuwa na uwezo wa kusoma baadhi ya taarifa zilizomfikia katika ofisi yake kwa ajili ya utekelezaji au kwa taarifa, hivyo basi taarifa nyingi alizokuwa nazo zilikuwa za wanafunzi, yaani mahudhurio, matokeo na nyinginezo zinazowahusu mwanafunzi.
“Jeshi lilipoanza uchunguzi wa makosa yake, kitu cha kwanza alikabidhi vitendea kazi vyake vyote kwa uongozi, hivyo hakuweza kutoroka na taarifa zozote za jeshi,” alisema Meja Komba.
Wakati JWTZ likitoa kauli hiyo, wiki iliyopita gazeti hili kupitia vyanzo vyake hivyo vya habari, vilimtaja ofisa huyo kuwa ni mmoja wa makachero wenye asili ya Rwanda waliokuwa wakifanya kazi ndani ya jeshi na ambao wanahofiwa kuwa watu wenye mawasiliano ya karibu na Serikali ya Kigali kwa malengo ambayo bado hayajawekwa bayana na kwamba alikuwa ametorokea nchini humo.
Gazeti hili kupitia vyanzo vyake vya habari, lilidokezwa kuwa kabla ya kutoweka, ofisa huyo ambaye nyendo zake zimekuwa katika darubini kali za makachero wa JWTZ, alikuwa akifanya kazi katika Kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano ya Kijeshi (IT), taarifa ambazo pia zimethibitishwa jana na JWTZ wakati wakilitolea ufafanuzi suala hilo.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment