HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled »  CHADEMA YADINDA; YARUKA KIHUNZI CHA HUJUMA ZA CCM ‘KUMTUMIA’ ZITTO

JITIHADA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mzozo kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zinaelekea kugonga mwamba.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya kutosha katika hujuma dhidi ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani wa chama hicho kuunda mgogoro na kukipasua.
Hata hivyo, licha ya misukosuko na kelele kutoka kwa baadhi ya wanachama na wanaodhaniwa kuwa ‘mapandikizi’, CHADEMA kimeweza kupuuza hujuma hizo na kujikita katika harakati za ujenzi wa ngazi za chini za chama katika vijiji na vitongoji.
Kwa sasa viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika majimbo 103 nchi nzima kujenga chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu lililoketi mwishoni mwa mwaka jana, kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko, na ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi unaokuja.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

Baadhi ya wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali wamekuwa wanashirikiana na wana CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya CHADEMA mtandaoni na mitaani. Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango na kuyapeperusha katika mikutano inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Kitila amevuliwa wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba amevuliwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ‘usaliti’.
Katika kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama wamekuwa wakitoa matamko, huku wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika mikoa ya Lindi na Singida.
Huku wakitoa shinikizo kwa chama Zitto asichukuliwe hatua zaidi, baadhi yao mkoani Kigoma walikwenda mbali wakitaka chama kiahirishe ziara ya Dk. Slaa mkoani humo hadi baadaye, kwa kisingizio cha usalama.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisisitiza kuwa masuala ya usalama yamezingatiwa barabara, na kwamba ziara ziko pale pale, kwani hakuna mkoa au wilaya ya mtu.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa uongozi wa CCM mkoani Kigoma, chini ya Dk. Aman Walid Kabourou, umekuwa ukiratibu vitisho na fujo katika mikutano au maeneo anayotembelea Dk. Slaa kwa lengo la kutisha wananchi.
Dk. Kabourou aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya CHADEMA kabla ya kukimbilia CCM miaka kadhaa iliyopita. Alipohamia CCM akapewa ubunge wa Afrika Mashariki. Sasa ndiye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.
Makundi ya vijana wa CCM na wana CHADEMA wenye matatizo na chama, wamekuwa wakisambazwa kuelekea maeneo kadhaa kwa lengo la kuhujumu mikutano ya Dk. Slaa.
Lengo ni kutumia fursa hii kujaribu kudhoofisha uwezo wa chama kinachohatarisha utawala wa CCM.
Miongoni mwa mikakati ya kuivuruga CHADEMA inayofadhiliwa kwa gharama kubwa ni kuwapandikiza vijana kufanya fujo katika mikutano ya Dk. Slaa.
Katika mikutano hiyo vijana mbalimbali wamekuwa wakijitokeza na mabango ya kupinga uamuzi wa kuondolewa kwa Zitto, kuzomea na kufanya vituko vyenye lengo la kuharibu mikutano hiyo.
Miongoni mwa matukio hayo ni lile lililotokea juzi katika Kijiji cha Mabamba  wilayani Kibondo, ambako zaidi ya vijana saba walikamatwa na kufikishwa kwenye kituo cha polisi.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwapo eneo la tukio waliwatambua kuwa wengi wao ni vijana wa CCM ambao wamekuwa wakizunguka katika mikutano yote anayofanya Dk. Slaa.
Katika mikutano yake mkoani Shinyanga na Kigoma, Dk Slaa, alisema propaganda za udini, ukabila na ugaidi zinazopandikizwa na CCM zimezidi kuimarisha chama chake katika safari ya kuelekea Ikulu mwaka 2015.
Dk. Slaa alisema wanaosema CHADEMA itakufa hawajui kinachoendelea, kwa sababu ya uamuzi wa kuwachukulia hatua au kuwaondolea nyadhifa watu wasiotaka kufuata maadili, katiba na miongozo ni njia ya kukipa uhai chama hicho.
“Mimi nilidhani CCM wangeshangilia chama chetu kufa, lakini hiki ninachokiona kinanistaajabisha; yaani eti wanatuonea huruma sisi tusife? Huu ni muujiza,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, limekuwa likidokezwa kuwa viongozi wa CCM wamekuwa wakifadhili harakati za kuidhoofisha CHADEMA ili wasipate upinzani mkali katika uchaguzi ujao.
Wiki iliyopita kupitia ukurasa wake wa facebook, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (bara), Mwigulu Nchemba aliandika kuwaMkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila aliyekuwa Kigoma alipigwa na wafuasi wa Zitto hadi kushindwa kusimama hadi aliposaidiwa na polisi.
Wakati Mwigulu akituma maneno hayo kupitia ukurasa wake, Kigaila amesema kuwa yeye yupo katika ziara ya kujenga chama mkoani Mbeya, na aliondoka Tukuyu kwenda Njombe kwa kazi hiyo hiyo.
Wakati wana CCM wakishangilia kile kinachoitwa mpasuko ndani ya CHADEMA, Dk. Slaa anasema wanazidi kuimarika na watafanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo.
Katika mazungumzo yake na Tanzania Daima, wiki iliyopita, Dk. Slaa aliwataka Watanzania wawe makini, kwani hao wanaotoa matamko ya kulaani Kamati Kuu wanafanya kazi ya CCM, hata kama baadhi yao wana kadi za CHADEMA.
“Wanaojitokeza kutoa matamko kulaani Kamati Kuu ya CHADEMA hawazungumzi bei ya umeme kupanda, hawazungumzi hali mbaya ya elimu na afya nchini, hawazungumzii suala la mishahara ya wafanyakazi, wamejikita kumjadili Mbowe na Slaa.
“Niwahakikishie wanachama na Watanzania wanaotaka mabadiliko kuwa tuna usalama uliokomaa tunajua hujuma zote, ndio maana jana Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, aliwatangazia Watanzania kuwa Mkurugenzi wetu wa Oganaizesheni na Mafunzo Benson Kigaila amepigwa na wafuasi wa Zitto na amesaidiwa na polisi wala hajiwezi hata kusimama.”
Dk. Slaa alisema wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa chama hicho wapo kwenye majimbo 103 nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa chama ngazi ya msingi, kutekeleza uamuzi wa Baraza Kuu. Alisisitiza kuwa ziara hizo hazina uhusiano na propaganda zinazosambazwa sasa kuhusu hatua ya chama hicho kumvua vyeo Zitto.
TANZANIA DAIMA

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: