Tangu karne nyingi, limau linajulikana kama dawa, husaidia pia kuongeza kinga ya mwili, kusafisha tumbo na hujulikana pia kwa kazi yake nzuri ya kusafisha damu. Limau ni matunda ambayo yana kitu muhimu sana katika kuondoa sumu mwilini kiitwacho kwa kitaalamu kama “flavonoids” ambacho chenyewe ni nyeti katika kupigana na kansa mbalimbali mwilini.
Juisi ya limau ina faida kadhaa nyingi kama vile kuondoa mchanga katika figo, kupunguza kukakamaa kwa mishipa (strokes) na kupunguza joto la mwili. Kama kinywaji ambacho huondoa uchovu mwilini, juisi ya limau itakusaidia kubaki mtulivu na mpole.Faida nyingi za limau zinatokana na virutubishi vyake vingi muhimu kama vile vitamini C, vitamini B6, vitamini A, vitamini E, folate, niacin thiamin, riboflavin, pantothenic acid, shaba, kalsiamu, chuma, magnesium, potassium, zinki, phosphorus na protini.Utafiti uliofanywa na Chama cha Madaktari wa magonjwa ya mfumo wa mkojo cha Marekani (American Urological Association), unaonyesha kuwa juisi ya limau au ‘lemonade’ inaweza kuondoa au kuzuia kujitokeza kwa mawe kwenye figo.
Zifuatazo ni faida mbalimbali za limau mwilini:
1. Kufunga choo na tumbo kushindwa kumeng’enya chakula
Juisi ya limau husaidia kutibu matatizo yahusianayo na tumbo kushindwa kumeng’enya chakula na kufunga choo. Ongeza matone machache ya limau kwenye chakula chako (kuwa makini sababu limau huwa haipatani na maziwa), na itakusaidia katika kumeng’enya chakula.
Unaweza pia kuongeza majani kidogo ya mnanaa (mint) na mbegu za shamari (fennel seeds) ili kuongezea ladha na harufu nzuri. Kunywa juisi hii kila unapokuwa umepata chakula cha mchana cha nguvu au cha jioni.
2. Hutibu homa
Juisi ya limau inaweza kumtibu mtu anayesumbuliwa na homa, mafua au baridi. Limau husaidia kutibu homa kutokana na sifa yake ya kuongeza kiasi cha jasho mwilini.
3. Huongeza afya ya meno
Juisi ya limau mara nyingi imetumika katika kulinda afya ya meno. Kama juisi fresh ya limau itanyunyizwa juu ya jino linalouma inaweza kusaidia kuondoa maumivu. Kusugua (masaji) juisi ya limau juu ya fizi za meno kunaweza kusaidia watu wenye matatizo ya kutokwa damu kwenye fizi huku ikiondoa harufu mbaya katika fizi na mdomo kwa ujumla.
4. Hutunza nywele
Juisi ya limau imejidhihirisha yenyewe kuwa dawa nzuri kwa upande wa matatizo mbalimbali ya nywele. Juisi ya limau ikipakwa kwenye ngozi ya kichwa inaweza kutibu matatizo kama ya mba, kupotea au kukatika kwa nywele, na matatizo mengine yahusuyo nywele na ngozi ya kichwa.
Kama utakuwa ukisafisha nywele zako kwa kutumia juisi au maji ya limau moja kwa moja basi utazifanya nywele zako zipate mng’aro wake wa asili bila gharama yoyote ya ziada.
5. Hulinda ngozi
Kwakuwa Juisi ya limau ni dawa ya asili dhidi ya bakteria, inaweza pia kutibu matatizo mbalimbali ya ngozi. Juisi ya limau inaweza kutumika kupunguza maumivu kwenye ngozi sababu ya kuungua na jua, pia husaidia kupunguza maumivu kutokana na kung’atwa na nyuki. Juisi ya limau au majimaji ya limau yanaweza kutumika kupakaa juu ya ngozi na kutibu chunusi na ukurutu.
Kunywa maji ya limau yaliyochanganywa na asali kunasaidia ngozi kuwa na afya zaidi na hata ukipekuwa huko sokoni utazipata baadhi ya sabuni ambazo zimetengenezwa kutokana na limau.
6. Hutibu majeraha ya moto
Upakaji wa maji ya limau (juisi) kwenye eneo la ngozi lililoungua huweza kusaidia makovu kupotea na hii husaidia pia kwa mtu aliyepatwa na malengelenge au vipele vyenye maji maji yanayouma ndani. Na kwa sababu limau ni wakala wa kupooza au wakala mtulizaji (cooling agent), huweza kupunguza maumivu au kuhisi kuungua kwenye ngozi hasa wakati unakuwa na majeraha yanayounguza ngozi.
7. Huzuia kuvujika kwa damu
Limau inayo sifa ya kudhibiti bakteria mwilini (antiseptic properties) na kugandisha damu, sifa hizi au kazi hizi mbili za limau husaidia kusimamisha kuvuja kwa damu ndani ya mwili. Unaweza kutumia maji ya limau ukiweka kwenye kipande cha pamba na kuiweke puani kuzuia pua kuvuja damu.
8. Hupunguza Uzito
Ikiwa utakunywa juisi ya limau iliyochanganywa na asali na maji ya uvuguuvugu, hasa asubuhi tu unapoamka inaweza kusaidia kupunguza uzito.
9. Hutibu matatizo kwenye mfumo wa upumuwaji
Juisi ya limau husaidia katika kutuliza matatizo katika mfumo wa upumuwaji kama vile pumu. Kwakuwa limau ina kiasi kingi cha vitamini C, husaidia kutibu na kutuliza matatizo ya muda mrefu kwenye mfumo wa upumuwaji.
Zingatia
Hutuliza maumivu ya miguu,Hutibu malengelenge (Corns),Hutibu maambukizi ya kwenye koo na Hutibu shinikizo la juu la damu. Hakikisha unakunywa robo Lita kutwa mara 2 kwa siku 10 kwa mtu mzima na glasi ndogo moja kwa siku kwa mtoto wa miaka miwili mpaka kumi.
Chanzo: Dk.Fadhili Paulo
Picha kwa hisani ya Mtandao
No comments:
Post a Comment