Kuna
msemo unaosema kuwa, “Afya ni mtaji”, ukiwa na maana kuwa, mtu unapokuwa
na afya nzuri ni tayari unakuwa na uwezo wa kufanya au kujihusisha na
kazi tofauti tofauti katika jamii na kupata matokeo yenye ufanisi, kwani
mwili wako, akili na roho yako vipo katika hali ya uimara wa kutosha.
Kwa
sababu ambazo yawezekana zikawa ndani au nje ya uwezo wa mtu, wengi wetu
tunajisahau kuwa, bila kuwa na afya imara hakuna kitu ambacho mtu
utaweza kukifanya kwa ufanisi. Badala yake tumekuwa tunafanya kazi zetu
za kila siku bila ya kuzingatia au kuchukua tahadhari dhidi ya hatari za
kiafya zinazoweza kumpata mtu kutokana na mazingira ya kazi
anazozifanya.
Mazingira ya kazi hutofautiana kwa mtu na mtu, pia hatari za kiafya zinatofautiana kwa kazi na kazi.
Ni wewe
ndiye unayefahamu kuwa unafanya kazi zako katika mazingira gani, ila
inawezekana ukawa hujafahamu kuwa mazingira ya kazi zako yana hatari
zipi za kiafya, au unazifahamu hatari za kiafya ila hufahamu njia salama
zaidi za kujilinda dhidi ya hatari hizo.
Kutokana
na kazi tunazozifanya kila siku, baadhi ya vitu ambavyo vinapatikana
katika mazingira ya kazi ambavyo ni hatari kwa afya zetu ni kama vile,
vumbi (la vyuma, mbao) kemikali mbalimbali, joto (la jua, moto),
bacteria (zaidi sana sehemu za kutolea huduma za afya), kutokana na aina
ya kazi inawezekana ukaufanyisha mwili kazi kubwa zaidi kuliko uwezo
wake, hatari za kuumia, kupata msongo wa mawazo na kuumia kisaikolojia
na pia inawezekana mazingira ya kazi yakakufanya mwili wako
usichangamke. Hivyo ni baadhi ya vitu au mazingira ya kazi ambayo
tunatakiwa kuyachukulia tahadhari ili tuendelee kuzilinda afya zetu.
Miongoni
mwa magonjwa ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kutegemeana na mazingira
ya kazi ni kama vile, magonjwa ya mapafu ikiwemo kansa, kansa za ngozi,
magonjwa ya akili, upofu, magonjwa ya moyo na kisukari pamoja na kulemaa
viungo vya mwili.
Baadhi
ya tahadhari ambazo tunaweza kuzichukua ili kujilinda na tuweze
kuendelea kufanya kazi katika hali ya usalama wa afya zetu zaidi ni kama
vile, kuzingatia mavazi ya kazi (mfano katika ujenzi, migodi,
mashambani au viwandani), kupata chanjo au dawa kutegemeana na aina ya
vijidudu hatarishi, kufanya mazoezi (kuuchangamsha mwili ili kuepukana
na hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kisukari, kuichangamsha akili),
kuuruhusu mwili upumzike, pia ni vyema ukaonana na mtu mwenye utaalamu
zaidi ili akushauri endapo kuna jambo ambalo linakutatiza ili uweze
kujilinda ipasavyo.
Kumbuka
ya kuwa, mtu wa kwanza mwenye wajibu wa kuilinda afya yako, ni wewe
mwenyewe. Chukua muda wa kutafakari kuwa, unafanya kazi katika mazingira
gani, kisha chukua hatua za kuilinda afya yako ili kazi yako uweze
kuendelea kuifanya kwa ufanisi zaidi.
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
No comments:
Post a Comment