Watafiti wa magonjwa wanadai kuwa msongo mkali wa mawazo wakati wa ujauzito unaweza kusababisha hitilafu katika uumbaji wa mtoto na hatimaye mtoto kuzaliwa akiwa mlemavu.
Ripoti
ya watafiti hao inazidi kuthibitisha matokeo ya tafiti zilizopita kuwa
mama mwenye msongo wa mawazo wakati wa ujauzito kutokana na mambo kama
kufukuzwa au kuachishwa kazi, kutengana na mwenza wake au kufiwa ana
hatari ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu kama vile midomo sungura (cleft lip na cleft palate) au matatizo kwenye uti wa mgongo (spina bifida).
Jopo
la watafiti wa kidenmark likiongozwa na Dr Dorthe Hansen walifanya
uchunguzi ili kuthibiitisha ukweli na uhakika wa dhana hii.
Wakitumia
rikodi za taarifa za kitabibu za kipindi cha miaka 12 kutoka 1980 mpaka
1992 kutoka masjala ya Taifa ya kitabibu, watafiti hao waliweza
kuwatambua wajawazito wote waliokumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha
wakati wa ujauzito na hata miezi 16 kabla ya kupata ujauzito. Matatizo
makubwa ya kimaisha yaliyochunguzwa yalikuwa kukumbwa na msiba wa ndugu
au jamaa wa karibu, ndugu au jamaa wa karibu kulazwa hospitali kwa mara
ya kwanza baada ya kugundulika kuwa na kansa ya aina yeyote au ndugu au
jamaa wa karibu kupatwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Mambo haya
yalichunguzwa kwa kigezo kuwa, mjamzito yeyote aliyewahi kukumbana nayo
ana hatari kubwa ya kuwa katika msongo wa mawazo bila kujali tabia yake,
kama ana watu wa kumfariji au uwezo wake wa kukabiliana nayo.
Jopo
hilo lilichunguza maendeleo ya mimba kwa wajawazito 3,560 ambao
walikumbana na matukio hayo kwa kulinganisha na wajawazito wengine
20,299 ambao hawakukumbana na hali yeyote ambayo ingewasababishia kupata
msongo wa mawazo wakati waujauzito.
Matokeo
ya uchunguzi wao yalionesha kuwa ulemavu na hitilafu za viungo kwa
watoto waliozaliwa ulikuwa mara mbili miongoni mwa kundi la wajawazito
waliokumbwa na msongo mkali wa mawazo ikilinganishwa na kundi la
kinamama ambao hawakuwa na hali hiyo.
Kadhalika ilionekana kuwa
wanawake waliowahi kukumbwa na hali kama hiyo katika ujauzito mbili
mfululizo za nyuma walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuzaa watoto
wenye ulemavu wa viungo tofauti na wale waliowahi kupatwa na hali hiyo
mara moja tu au wale ambao hawakupatwa kabisa.
Ilionekana pia
kuwa tukio lililoongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa
viungo ilikuwa ni iwapo mjamzito atafiwa na mtoto wake mwingine mkubwa
wakati akiwa katika miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito wake huu wa sasa.
Hatari ya kuzaa mtoto mlemavu iliongezeka iwapo kifo cha mtoto huyo
mkubwa kingetokea bila kutarajiwa kwa mfano kwa ajali.
Watafiti
wanasema kwamba, msongo mkali wa mawazo huchangia kuathiri uumbaji wa
mtoto aliye tumboni kwa kusisimua uzalishaji wa homoni ya cortisone.
Homoni hii husababisha ongezeko la kiwango cha sukari katika damu na
upungufu wa usambazaji wa hewa safi ya oksijeni kwa mtoto, mambo ambayo
husababisha kutokea kwa hitilafu katika uumbaji wa viungo vya mtoto
hatimaye kusababisha ulemavu wa viungo vya mtoto.
Uwezekano
mwingine ni kuwa msongo mkali wa mawazo humchochea mama mjamzito kutumia
zaidi vileo vyenye alcohol na pia kula lishe duni hali ambayo huongeza
madhara zaidi kwa kiumbe kilicho tumboni.
Hata hivyo Professor Peter Hepper wa Chuo Kikuu cha Queen's cha Belfast, anasema hakushangazwa na mtokeo ya utafiti huo.
Anasema
kuwa, "tunafahamu msongo wa mawazo husababisha mabadiliko ya
kifiziolojia katika mfumo wa mwili wa mjamzito, na hivyo hakuna sababu
kwanini mabadiliko hayo yasimfikie pia mtoto aliye tumboni kupitia kondo
la nyuma na kumuathiri. Matokeo haya yanazidi kuthibitisha kile
tulichokuwa tukikifahamu tangu awali kuwa msongo wa mawazo wa muda mrefu
kwa mwanamke una madhara makubwa kwa mendeleo ya uumbaji wa mtoto aliye
tumboni na hivyo basi hakuna budi kufanyike kila njia kuwasaidia
wajawazito walio katika hali hii ili waweze kujifungua watoto walio na
afya njema na salama."
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG




No comments:
Post a Comment