Ni kawaida watoto wadogo kunyonya kidole kutokana na
mahitaji ya kimwili na kisaikolojia. Mtoto huanza kunyonya kidole endapo
hapati maziwa ya kutosha. Mara nyingine husababishwa na matatizo ya
kihisia.
Kwa mtoto, kunyonya kidole ni namna ya
kujifariji. Mtoto asipotosheka kila anaponyonya huanza kunyonya kidole
ambako humfanya apunguze njaa. Kisaikolojia; hujibembeleza na kujisikia
salama.
Mara nyingi mtoto ataacha kunyonya kidole akiwa na
umri kati ya miaka mitatu mpaka sita, ingawa wengine huendelea hadi ukubwani.
Inasemekana kuwa tabia hii huanzia tumboni baada ya
wiki kumi na tatu za ujauzito na huendelea mpaka motto anapozaliwa ingawa
wazazi wengi hugundua hilo mtoto anapofikisha umri wa miezi miwili mpaka mitatu.
Zipo faida zilizothibitika za watoto kunyonya
kidole. Nyingine zinaendelea kuchunguzwa. Baadhi ya watafiti
wanadai unyonyaji huo huimarisha kinga ya mwili. Watafiti hao wanadai
unyonyaji wa dole gumba na ung’ataji wa kucha husaidia kuzuia mzio au allergy.
Hasara
Kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote, hili nalo
linalo hasara zake. Zipo zitokanazo na mtazamo na imani za jamii husika
na zile za kimuonekano.
Kwenye jamii zilizopo, baadhi ya watu huamini mtoto anayenyonya
kidole anajipunguzia uwezo wa kuzingatia masomo, hivyo kuwa mjinga jambo ambalo
halijathibitika.
Upo uwezekano wa mdomo hasa kuathirika. Inaelezwa
kuwa zinaweza kulegea kutokana na uzito wa kidole sambamba na mtoto
kuchelewa kuwa na ufahamu kutokana hutumia muda mwingi kunyonya kidole.
Wazazi wanashauriwa kuwa macho ili kunusuru hali hii.
Endapo mtoto ataendelea kunyonya hata akiwa na umri
mkubwa kidogo inaweza kusababisha meno kutojipanga vizuri kwenye fizi.
Madaktari wa kinywa wamehusisha mpangilio mbaya wa meno na kunyonya kidole hasa
gumba, kwani meno husukumwa kwenda mbele au kujipanga vibaya na hivyo kuathiri
muonekano wa mhusika.
Daktari bingwa wa meno, Christopher Ruhinda wa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anathibitisha hili. Ni
kweli. Nguvu (presha) anayotumia mtoto kunyonya kidole inaharibu
mpangilio wa meno. Mara nyingi yanatoka nje na mdomo hushindwa
kufunga,anasema Dk Ruhinda.
Kunyonya kidole sio hatari ikiwa mtoto ataacha kabla
ya miaka mitano. Kama mtoto atashindwa kuacha kunyonya kidole mpaka baada
ya umri huo kuna uwezekano wa meno yake kutojipanga vizuri na kuota yakiwa
yamebebana au kuwa na meno yasiyokutana.
Watoto wanaonyonya kidole baada ya miaka minne au
mitano wana hatari ya kupata tatizo hili hivyo kuathiri muonekano wao wa sura
na hata matatizo ya kuongea vizuri. Hii huweza kutokea kutokana na
kulegea kwa lips ambazo ni muhimu kwa matamshi ya baadhi ya maneno. Meno
yaliyokosa nafasi au yenye nafasi kubwa nayo yana athari kwenye matamshi.
Kutokana na kunyonya huko mtoto atapata tatizo la matamshi na viungo vya mdomo
mfano ulimi kutoka nje wakati wa kuongea.
Inategemea na ukubwa wa athari. Kama mpangilio
haujawa mkubwa sana mpangilio mbaya huweza kujirekebisha wenyewe iwapo mtoto
ataacha kunyonya kidole. Kwa wale wanaopitiliza wanahitaji huduma za
mtaalamu wa meno (orthodontist) kufanya marekebisho.
Ipo mifano kadhaa ya watu waliowahi kufanya upasuaji
wa fizi ili kurekebisha mpangilio wa meno kuupata muonekano wanaouhitaji.
Cha kufanya
Inashauriwa kutomkataza mtoto kunyonya kidole akiwa
chini ya miaka minne au mitano isipokuwa kama kuna tatizo linalojitokeza au
mtoto akianza ghafla kufanya, hivyo baada ya miezi kumi tangu azaliwe na
ikiambatana na kuvuta nywele.
Ili kupunguza uwezekano huo, mama anayenyonyesha
anapaswa kula vyakula vyenye lishe kamili vitakavyosaidia mwili kutengeneza
maziwa ya kutosha kumnyonyesha na kumshibisha mtoto kila wakati, hivyo kumuepusha
kunyonya kidole.
Kwa mtoto anayenyonya, wazazi au walezi wanapaswa
kumueleza kwa upole wakitumia lugha laini ikibidi kumuahidi zawadi nzuri ili
akubali kuacha kunyonya kidole.
Kumuanzisha shule ni njia nyingine inayoweza kumsaidia
mtoto kuacha kunyonya kidole. Shule kutamfanya aone aibu hasa atakapokuwa
anataniwa na wenzake anaosoma na kucheza nao.
Njia mbadala pia zinaweza zikatumika. Hizi
zitamsaidia kuacha mapema zaidi. Kupaka pilipili vidole vyake ili
akinyonya awashwe na ukali wa atakaokutana nao itamfanya asirudie tena kufanya
hivyo ingawa kutakuwa na jukumu la kubembeleza atakapokuwa analia baada ya
kunyonya kidole.
Kushiriki michezo inayoshughulisha mikono kwa muda
mwingi ni njia nyingine ya kufanikisha suala hili. Unaweza ukampa midoli
au wanasesere, au acheze na wenzake ili mradi viganja vyake viwe na shughuli ya
kufanya na kumnyima nafasi ya kunyonya kidole.
Pia, unaweza kumnunulia nyonyo za plastiki ili umpe
anyonye badala ya kidole. Hii itamfanya asipate muda wa kuzoea kunyonya
kidole na hatotumia muda mwingi kunyonya nyonyo hizo.
Wengine kuwavalisha watoto mipira ya mikono au viganja
(gloves) na kuwafanya washindwe kunyonya vidole.
Iwapo vyote vitashindikana basi mzazi au mlezi asisite
kuwaona madaktari wa afya ya meno na kinywa kwa msaada zaidi.
No comments:
Post a Comment