Baadhi
ya maswali tuliyopokea, mengi yalihusu maradhi ya sunzua ambayo
kitaalmu yanajulikana kama warts. Sunzua ni ugonjwa wa ngozi
unaofahamika na wengi. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo
kitaalamu huitwa humanpapilloma virus.
Karibu
asilimia 10 ya wanadamu wamewahi kupata athari za virusi vya ugonjwa
huu, achilia mbali kuumwa sunzua. Kwa sababu hiyo ndiyo kusema kila mtu
anapaswa kufahamu ugonjwa huu kwa undani ili unapojitokeza awahi
hospitali ili kuudhibiti.
Virusi
vinavyosababisha ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda
kwa mwingine kwa njia ya ngono.Ugonjwa huu hutokea sehemu mbalimbali za
mwili, lakini huwatokea wengi sehemu za siri.
Sunzua kama
ugonjwa wa zinaa, huathiri sehemu za siri pamoja na njia ya haja kubwa.
Wagonjwa ambao wanaishi na Virusi vya Ukimwi wako kwenye mazingira
hatarishi zaidi ya kupata sunzua.
Virusi vinavyosababisha maradhi ya sunzua huambukizwa
kwa njia ya ngono na ni mara chache huweza kusambaa kwa njia ya
kugusana. Virusi wa maradhi haya wanajulikana kama papilloma na
hujitokeza kwenye eneo la ngozi ambapo virusi hivi vimepenya. Mara
nyingi hujipachika kwenye mchubuko au mpasuko wa ngozi.
Maradhi
haya huweza kujitokeza kwenye ngozi kati ya miezi miwili hadi tisa
baada ya kupenya kwenye ngozi.Maradhi haya husababisha ngozi kutokuwa na
muonekano wake wa kawaida Husababisha ngozi kuwa na milima na mabonde
kiasi cha kusababisha kukatika kwa urahisi na kufanya virusi kuendelea
kupenya.
Dalili za maradhi haya ni kuwa na ngozi iliyoinuka, iliyopoteza unyoofu wake na yenye muonekano mfano wa maua. Sunzua ziko za aina tofauti kulingana na mahali ugonjwa unatokea na kuonekana kuiathiri ngozi.
Sunzua ya sehemu za siri au kwa kitaalamu condyloma acuminatum (venereal warts).
Aina
hii ya ugonjwa kwa wanawake huathiri sehemu za nje za maumbile ya siri
na mara nyingine huweza kujitokeza na kuathiri shingo ya kizazi. Kwa
wanaumesunzua huathiri uume wenyewe, korodani, nyonga mpaka kwenye mapaja.
Sunzua
hii ya sehemu za siri kwa watu wa jinsia zote hujitokeza kama uvimbe
ulioinuka au zikawa sawia bila uvimbe wa aina yoyote. Sunzua zinaweza
kuwa kubwa au ndogo, zikawa mojamoja au zikajikusanya pamoja kama
mafungu zikafanana kabisa na maua.
Huwa
zinaweza kutokea usoni, hasa sehemu karibu na kope ama maeneo mengine
kama vile vidole vya miguu na mikono. Sunzua huwa haziumi na sanasana
huwa zinawasha na huweza kujitokeza katika kipindi cha miezi miwili
mpaka tisa baada ya maambukizi ya virusi.
Kwa
wanawake, sunzua ya kwenye shingo ya kizazi huweza kusababisha saratani
ya shingo ya kizazi. Kwa sababu hiyo, mwanamke anapaswa kujichunguza
ili kuchukua hatua mwafaka za matibabu.
Ndugu
msomaji, kwa jumla magonjwa ya ngozi ni mengi na yanaathiri binadamu
kwa namna tofauti. Kama nilivyoeleza hapo awali, yanayotokana na
bakteria, fangasi, virusi na hitilafu nyingine katika damu au ngozi.
Tutaendelea
kujibu maswali mbalimbali ya wasomaji kulingana na mtakavyouliza. Kwa
wale ambao maswali hayakujibiwa wasikate tamaa kwani kadri tutakavyopata
nafasi, yataendelea kujibiwa.
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
IMEANDALIWA NA DOCTOR JOH BLOG
No comments:
Post a Comment