
Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi wa mwanamke
au ectopic pregnancy ni tatizo ambalo limetokea kuathiri
wanawake mbalimbali. Kwa kawaida, isipokuwa mara chache sana, mimba zitungazo
nje ya mfuko wa uzazi hazina uwezo wa kukua kuwa mtoto kamili.
Aidha, mimba hizi ni hatari kwa afya ya mama
mjamzito kwa vile humfanya kupoteza damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo.
Nini hutokea?
Kazi za mirija ya fallopian ni
kusafirisha mayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji (ovary)
mpaka kwenye mfuko wa uzazi (uterus). Utungisho wa yai la kike (ovum)
na mbegu ya kiume (sperm) hufanyika kwenye mirija hii.
Mara baada ya utungisho, misuli inayozunguka mirija ya fallopian
ikishirikiana na vinyweleo vilivyopo ndani ya mirija hii husukuma kiinitete au
yai lililorutubishwa kulipeleka kwenye uterus. Yai lililorutubishwa, au
kiinitete, lifikapo kwenye uterus hujipachika katika mojawapo ya kuta zake kwa
ajili ya kuendelea kurutubishwa, kukua taratibu na hatimaye kufanya mtoto.
Inapotokea misuli hii kushindwa kufanya kazi au vinyweleo hivi
kukosekana, kiinitete hushindwa kusafirishwa kuingia kwenye uterus na hivyo
hujitunga nje ya uterus kusababisha ectopic pregnancy. Karibu
asilimia 1-2% ya mayai yaliyorutubishwa hutunga nje ya mfuko wa uzazi wa
mwanamke.
Aidha, zaidi ya asilimia 95% ya mimba zinazotunga nje ya uterus hutokea
kwenye mrija wa fallopian. Mimba zinazotunga kwenye mrija wa fallopian
husababisha kiinitete (embryo) kujipachika katika kuta zake na hivyo
kusababisha mishipa ya damu inayopita karibu na mrija wa fallopian kupasuka na
damu kutoka kwa wingi hali ambayo isiposhughulikiwa mapema husababisha madhara
zaidi na hata kifo.
Aina za Ectopic Pregnancy
Kuna aina kuu nne za mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi, nazo ni
1. Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian
2. Mimba zinazotunga nje ya uterus na nje mirija ya fallopian
3. Mimba zinazotunga ndani na nje ya uterus kwa wakati mmoja
4. Mimba zinazojirudia kutunga nje ya mfuko wa Uzazi
Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian
Sababu kubwa inayopelekea mimba kutunga kwenye mirija ya fallopian ni
kushindwa kusafirishwa kwa kiinitete katika mirija hii hali inayotokana na
mabadiliko katika hali ya mirija au uwezo duni wa mirija hiyo katika kusukuma
kiinitete kuingia kwenye uterus kwa sababu ya ukosefu wa vinyweleo kutokana na
magonjwa mbalimbali yanayoathiri muundo na maumbile ya mirija ya fallopian.
Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian huwa zina madhara makubwa
zaidi kwa sababu eneo hili ni jembamba mno kuweza kuhimili ukuaji wa mimba na
pia lina mishipa mingi ya damu inayopita karibu ambayo ipo hatarini kupasuka
hivyo kupelekea mgonjwa kupoteza damu nyingi sana.
Mimba zinazotunga nje ya uterus na nje mirija ya fallopian
Baadhi ya mimba huweza kutunga kwenye kiwanda cha kuzalisha mayai (ovary),
kwenye shingo ya uzazi (cervix) au ndani ya tumbo (intra-abdominal).
Aina hii ya mimba ni chini ya asilimia tano ya mimba zote zinazotunga nje ya
mfuko wa uzazi.
Mimba inayotungwa ndani ya tumbo (intra-abdominal) wakati fulani huweza
kutoa mtoto aliye hai tofauti na aina nyingine za mimba zinazotunga nje ya
uterus. Hata hivyo uzalishaji wake hufanywa kwa operesheni ingawa hakuna
ushahidi wa kitabibu kuhusu suala hili mpaka sasa.
Madhara ya kutokea kwa upotezaji wa damu pamoja na maambukizi ni makubwa
hivyo mara nyingi mimba za namna hii huitaji kushughulikiwa haraka ili
kumuepushia madhara makubwa mama mjamzito.
Mimba zinazotunga ndani na nje ya uterus kwa wakati mmoja
Wakati fulani, mayai mawili yaliyorutubishwa kwa wakati mmoja hutokea
kupandikizwa sehemu mbili tofauti. Moja likipandikizwa nje ya uterus na jingine
ndani ya uterus. Katika aina hii ya ectopic pregnancy, uwezekano wa yai
lililotungwa ndani ya uterus kukua na kutoa mtoto ni mkubwa sana.
Mimba zinazojirudia kutunga nje ya mfuko wa Uzazi
Wakati fulani hutokea kuwa, hata baada ya operesheni ya kuondoa mimba
iliyotunga nje ya kizazi kufanyika, baada ya muda fulani seli za kiinitete
huendelea kukua na kujitengeneza tena kufanya kusanyiko la seli kama mimba
nyingine. Hali hii huitwa mimba zinazoendelea kutunga nje ya mfuko wa uzazi
au persistent ectopic pregnancy.
Nini husababisha mimba kutunga nje ya kizazi?
Katika mimba nyingi zinazotunga nje ya uterus, chanzo chake huwa
hakijulikani. Hata hivyo kuna vihatarishi ambavyo humfanya mwanamke kuwa katika
hatari ya kupata tatizo hili. Vihatarishi hivi ni pamoja na
1. Matatizo katika mirija ya fallopian
Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na
· Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
· Matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba (Intra-uterine
contraceptive devices)
· Kuoteana kwa tishu za uterus kwenye viungo vingine
vya uzazi au endometriosis.
2. Uvutaji sigara
Uvutaji sigara kwa mwanamke una uhusiano mkubwa na utungaji wa mimba nje
ya kizazi. Imeonekana kwamba wanaowake wanaopendelea kuvuta sigara mara kwa
mara wana hatari ya kupatwa na tatizo hili mara tano zaidi ya wale wasiovuta
kabisa. Hali hii husababishwa na nicotini iliyomo ndani ya tumbaku. Kwa kawaida
nicotini huchochea kusinyaa kwa mirija ya fallopian hali iletayo kuziba kwa
mirija hiyo na hivyo kufanya kiinitete kushindwa kupita kwenye mirija kuingia
kwenye uterus na kufanya mimba kutunga kwenye mirija ya fallopian.
3. Upasuaji wa tumbo uliofanyika zamani
Operesheni yeyote inayohusu mirija ya fallopian inaongeza uwezekano wa
mwanamke kutunga mimba nje ya uterus kwa vile mirija ya fallopian huwa
imesinyaa kutokana na operesheni hiyo.
4. Matumizi holela ya baadhi ya dawa
Matumizi ya baadhi ya dawa zenye homoni husababisha kupungua kwa uwezo
wa mirija ya fallopian kusukuma kiinitete kuelekea kwenye uterus na hivyo
kuleta uwezekano wa utungaji wa mimba nje ya kizazi. Dawa hizo ni kama dawa za
kuzuia mimba zenye homoni za kike za progesterone, na dawa za kusaidia
uzazi aina ya clomiphene.
Dalili za ectopic pregnancy
Katika wiki za mwanzo za ujauzito, mimba iliyotunga nje ya uterus huwa
na dalili sawa na za mimba ya kawaida. Dalili hizi ni pamoja na mwanamke kukosa
hedhi, kujaa kwa matiti, kichefuchefu, na uchovu wa mwili. Hali hii hufanya
ugunduzi wa mimba iliyotunga nje ya uterus kuwa mgumu katika hatua zake za
awali.
Hata hivyo dalili ya awali ya kuonesha kuwa mimba imetunga nje ya kizazi
ni kuwepo kwa maumivu makali na damu kutoka ukeni. Maumivu yanaweza kuwa kwenye
nyonga, tumbo au wakati mwingine kwenye mabega au shingo (iwapo kiwango cha
damu inayotoka kwenye mirija iliyopasuka ni kingi sana mpaka kugusa kiwambo cha
hewa).
Maumivu haya huweza kuwa makali na yanayokata kama kisu, na yanaweza
kuwa upande mmoja zaidi wa nyonga ingawa si lazima yawe upande ulio na mimba.
Dalili nyingine ni pamoja na
· Kizunguzungu na kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu
kwa wingi
· Shinikizo la damu kuwa chini, na
· Maumivu ya chini ya mgongo
Ugunduzi wa ectopic pregnancy
Mimba iliyotungwa nje ya kizazi huweza kugunduliwa kwa
· Daktari kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu
dalili zake na kumfanyia uchunguzi wa mwili (physical examination).
·
· Kufanya vipimo kadhaa vinavyoonesha kuwepo kwa
tatizo hilo. Vipimo hivyo ni pamoja na
· Kupima damu kwa ajili ya kuangalia kiwango cha
homoni ya HCG
· Kupima kiwango cha homoni ya progesterone ambayo
kwa mama mwenye ectopic pregnancy huwa chini (chini ya 15ng/mls) zaidi ya
mwenye mimba ya kawaida.
· Ultrasound ambayo husaidia kutambua mimba
ilipotungwa.
Matibabu ya Ectopic pregnancy
Matibabu ya mimba iliyotunga nje ya kizazi yaweza kuwa ya aina mbili,
yale yasiyohitaji upasuaji, au yanayohitaji uangalizi na dawa na yale
yanayohitaji upasuaji.
1. Matibabu kwa kutumia dawa:
Faida kubwa ya kufanya uchunguzi mapema ni kuwa inaongeza uwezekano wa
kuokoa maisha ya mama, kuokoa mirija isipasuke na hivyo kuongeza uwezekano wa
kupata mimba kwa njia ya kawaida siku za usoni. Iwapo, mimba bado ni ndogo sana
na kiwango cha HCG bado kipo chini mno, daktari anaweza kushauri kusubiri huku
akimfuatilia mgonjwa kwa ukaribu sana. Wakati mwingine, mwili huwa na uwezo wa
kuifyonza mimba changa ndani kwa ndani na hivyo kuondoa hatari ya kuwepo kwa
ectopic pregnancy.
Hali kadhalika, mama anaweza kupewa dawa aina ya methotrexate, ambayo
ina uwezo wa kuzuia mimba kukua zaidi. Wakati dawa hii inapotolewa, ni muhimu
pia kufuatilia kiwango cha HCG ili kujiridhisha kuwa kimeshuka mpaka kufikia
sifuri ili kuwa na uhakika kuwa mimba haipo tena.
Baadhi ya madaktari pia hutumia njia ya kuchoma dawa ya sumu ya
potassium chloride kwenye mimba ili kuifanya isinyae na hatamaye kufyonzwa na
mwili. Matibabu haya hufanyika chini ya uangalizi wa kipimo cha ultrasound.
2. Matibabu kwa kutumia upasuaji
Iwapo mrija tayari umepasuka, upasuaji wa dharura hufanyika kwa ajili ya
kuzuia kupotea zaidi kwa damu. Sehemu ya mrija iliyopasuka huondolewa na mshipa
wa damu uliopasuka hufungwa. Athari za matibabu kwa njia hii ni kuwa, huondoa
uwezo wa mrija ulioathirika kupitisha yai tena maishani na hivyo kupunguza
uwezekano wa mama kupata mimba siku za usoni.
Njia za kuzuia mimba kutunga nje ya kizazi
Yawezekana kupunguza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa kuzuia
na kujiepusha na vihatarishi vinavyosababisha hali hiyo. Njia hizo ni kama
· Kujikinga na maambukizi katika mfumo wa uzazi wa
mwanamke kwa kujiepusha na ngono zembe, au kupunguza idadi ya wapenzi wa
kufanya nao ngono.
· Kuacha kutumia holela dawa za homoni bila kupata
ushauri wa daktari, na
· Kujiepusha na uvutaji wa sigara. Tatizo la
Mimba Kutunga Nje ya Mfuko wa Uzazi (Ectopic Pregnancy)
No comments:
Post a Comment