SIMBACHAWENE ATAKA WANANCHI KUTUNZA MIRADI YA TASAF



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewasihi wananchi kuthamini na kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika maeneo yao kwa kuwa ina lengo la kuondoa umaskini katika jamii.

Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na Wananchi kwa ujumla katika Halmashauri za Wilaya ya Geita, Chato na Bukombe Mkoa wa Geita.

“Nimetembelea na kukagua miradi iliyopangwa, kwa ujumla nimefurahi sana kwa utekelezaji mzuri mathalani shule na vituo vya afya vimejengwa kwa viwango vizuri. Hivyo, nitoe rai kwa halmashauri zote nchini na wananchi kuhakikisha miradi hiyo inatunzwa kwa kuwa ni sehemu ya chaguo na vipaumbele vya wananchi wenyewe katika maeneo yao” amesema Mhe. Simbachawene.

Aidha, simbachawene ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo mmoja ametoa fedha nyingi kupitia mpango huo ili ziwafike wanufaika na wananchi kwa jumla kupitia miradi hiyo ambayo ni chachu ya maendeleo.

Hivyo, ameomba wananchi kuendelea kumuombea ili aendelee kuwa na moyo wa huruma na unyenyekevu kwa maendeleao ya wananchi wake.

“Umaskini si kukosa fedha tu, unaweza pia kuwa ni ukosefu wa elimu na afya bora. Kwa kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtu wa maono amegusa sehemu hizo na kuhakikisha shule nzuri na vituo vya afya kama vilivyojengwa mkoani Geita kupitia Mradi huo vinakamilika haraka na kuanza kutumika” amesema Mhe. Simbachawene

Vilevile, Simbachawene amewasisitiza Waratibu wa TASAF katika Mkoa wa Geita kuhakikisha shule na vituo vya afya vinavyojengwa kupitia Mradi huo wa TASAF vinawekewa miundombinu ya maji na umeme na kuweka madawati ili madarasa hayo yaanze kutumika.

Waziri Simbachawene amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani Geita na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzitatua na kukagua miradi inayotekelezwa na TASAF katika Halmashauri za Geita, Chato na Bukombe katika Mkoa huo.

No comments

Powered by Blogger.