Sakata la gesi Mtwara, Baba wa Taifa akumbukwa
SAKATA la wakazi wa Mkoa wa Mtwara kupinga
rasilimali ya gesi ghafi asilia inayovunwa katika kijiji cha Msimbati
mkoani humo kupelekwa Dar es Salaam kwa njia ya bomba limepamba moto
huku viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakitumia hotuba na nukuu za
kauli za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuhamasisha wananchi
kumuenzi mwasisi huyo wa taifa kwa kuupinga mradi huo.
Katika mkutano mkubwa uliofanyika jana Mtaa wa
Sinani mjini hapa viongozi wa CUFWilaya ya Mtwara Mjini, walikuja na
mbinu mpya ya kuhamsisha wananchi kuendelea na msimamo huo kwa kutoa
hotuba za nukuu ya kauli za Baba wa Taifa kuhusu mustakabali wa hali ya
maisha ya wananchi katika mazingira ya wachache kuwakandamiza wengi.
Saidi Kulaga, Katibu wa CUF Wilaya ya Mtwara mjini
alisema kinachotokea leo kwa wakazi wa mikoa ya Kusini ni kumuenzi
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye kwa nyakati tofauti
alinukuliwa akionya viongozi kuandamiza wengi.
Katibu huyo akisoma karatasi ya nukuu hizo kutoka
katika kitabu cha ‘Reflection on Leadership in Africa’ kilichopigwa
chapa na VUB University Press, 2000 alisema mwasisi huyo wa Taifa
katika kitabu hicho amenukuliwa akisema
“Amini nawaambieni enyi Waswahili wachache
mnaotawala, mnategemea kweli kuwa mtawaongoza Watanzania kwa lazima
wakati wanapoteza matumaini na mtegemee kuwa watasalia wamekaa kimya kwa
amani na utulivu?”
Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu Kulaga
alisema “Sio mimi ni Mwalimu Nyerere anasema….wengi katika nchi zetu ni
wajinga ndiyo maana wanakubali kutawaliwa hivyo, kukubali kukandamizwa
namna hiyo wakati wanayo nguvu inayotokana na wingi wao, ni kwa sababu
ya ujinga tu, hivyo basi Watanzania watakuwa wajinga na mataahira
(idiots) kama watakubali kuendelea kukandamizwa na kikundi cha wachache
(viongozi) katika nchi yao wenyewe”.Katibu huyo alisema Nyerere katika
kitabu hicho anasema“Ni ukweli usiopingika kuwa masuala ya maendeleo
hayawezi kuwa masuala ya ubabaishaji tu na hakutakuwa na watu wa kizazi
hiki na karne hii ambao watatakiwa kujitoa muhanga kwa ajili ya maisha
bora katika siku chache zijazo wakakubali, wakati wanawaona watu
wachache wakiendelea kuneemeka machoni pao bila kujali wakati ujao,
wakati wao (wananchi) na watoto wao wakiendelea kuishi maisha duni na
dhalili”.
Alibainisha kuwa kwa kuwa Serikali imeshindwa
kuyaenzi maneno ya Mwalimu Nyerere wakazi wa Mtwara wamejitolea kuyaenzi
maneno hayo kwa vitendo na kwamba hakuna tone la gesi ghafi
litakalosafirishwa kwa njia ya bomba hadi Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa wananchi wanatambua wazi kuwa gesi
ni rasilimali ya Taifa lakini alihoji kwa nini Twiga wanaopatikana
katika hifadhi za Serengeti hawahamishiwi katika hifadhi za kusini
ilhali ni rasilimali ya Taifa?
“Naomba Tueleweke hatupingi gesi kunufaisha Taifa
ila tunapinga mitambo ya kufua umeme kujengwa Dar es Salaam , tunataka
mitambo na viwanda vijengwe Mtwara halafu faida itakayopatikana
ilinufaishe taifa” alifafanua Kulaga
Katibu huyo pia aliweka hotuba ya Nyerere
mkutanoni hapo inayopinga matumizi mabaya ya rasilimali za nchi kwa
kunufaisha wachache huku wengi wakiendelea kuteseka, kitendo hicho
kilivuta hisia za wengi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Cuf Taifa,
Katani Katani alisema uvumilivu wa watu wa kusini wa kudhulumiwa fursa
za maendeleo umefika mwisho na kwamba hawako tayari kuona gesi asilia
ambaye alilifananisha kama karata ya mwisho ikishindwa kuwakomboa.
“Tushikamane kwa hili, tuweke tofauti zetu
kando…tuiambie Serikali katika hili hapana…kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete
katika hotuba yake ya salamu za mwaka mpya amesema lazima gesi itaondoka
basi tunamweleza haiondoki ajiandae kwa hatua nyingine,” alisema Katani
huku akishangiliwa na vijana.
Tofauti na mikutano mingine mkutano huo ambao uliitishwa na Cuf
pekee, ulihutubiwa pia na kada wa CCM, Mzee Rashid Abdallah ambaye
aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kutetea maisha yao.
“Hii gesi siyo ya kwetu sisi wazee, uliwahi
kusikia maisha yanatafutwa uzeeni, tunataka gesi ibaki kwa ajili yenu na
watoto wenu….simamieni” alisema Mzee Abdallah huku akishangiliwa kwa
nguvu na wananchi waliofurika mkutanoni hapo.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment