Dowans kaa la moto;Mahakama ya Rufani yaiamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia

TANESCO 
 
Uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walikubaliana na hoja za pingamizi la Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama, kuwa maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda.
Dar es Salaam. Kufuatia Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kuzuia utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu iliyoliamuru liilipe fidia Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura, Dowans, wananchi wamehoji sababu ya Serikali kuzembea hadi deni hilo kuongezeka.
Tanesco iliwasilisha katika Mahakama ya Rufani maombi ya kusimamisha utekelezwaji wa hukumu ya Mahakama Kuu, ikidai kuwa Dola za Marekani 65 milioni, walizoamriwa na ICC kuilipa Dowans ni kiasi kikubwa, endapo kitalipwa Tanesco itapata hasara kiuchumi.
Tanesco iliongeza kuwa kama mchakato wa utekelezaji wa hukumu hiyo utaendelea, utaathiri uwezo wake wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini na hivyo kusababisha tatizo kubwa la ukosefu wa umeme, ambao utaathiri uchumi wa nchi kwa jumla.
Hata hivyo, wakati hukumu ya sasa inatolewa riba ya deni hilo imeongezeka hadi kufikia dola 122 milioni ikiwa ni ongezeko la dola 58 milioni.
Wakizungumzia ongezeko hilo baadhi ya wanasiasa wameilaumu Serikali kwa kuzembea hadi deni hilo  kufikia kiasi hicho.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema kuwa hasara hiyo inatokana na wanasiasa na wataalamu wa Serikali kulazimisha kuvunjwa kwa mkataba wa Dowans badala ya kusubiri muda wake uishe.
“Walifanya haraka kuvunja mkataba wakati ilikuwa imebaki miezi mitatu tu uishe. Kulikuwa na wanasiasa na wataalamu wetu walioshinikiza mkataba uvunjwe na hayo ndiyo matokeo yake,” alisema Keissy.
Naye Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ameilaumu Serikali kwa kutokuwa makini inapoingia mikataba.
“Mambo ya mikataba ni ya kisheria kati ya pande mbili. Lazima kuwe na umakini, kwanza ujue nia ya kuingia mkataba, matazamio na faida zake. Lazima pia kuwe na elimu kwa wataalamu wetu,” alisema Mbatia na kuongeza;
“Hapa Serikali imekosa umakini ndiyo maana tumeingia kwenye hasara kama hiyo. Kwa sasa siwezi kusema hatua gani ichukuliwe kwa sababu sijaiona hukumu lakini huo ni uzembe.”
Naye Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany alisema hayo ndiyo matokeo ya Serikali kutokuwa makini na mikataba.
“Sisi kama wabunge tuliipigia mno kelele Serikali bungeni na hata Mwenyekiti wetu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alishasema, hakutakuwa na mafanikio hata kama itakata rufaa. Sasa ndiyo yametokea. Sasa huu ni mzigo watakaobebeshwa wananchi,” alisema Barwany na kuongeza:
“Kama wabunge tunapendekeza kuwa mikataba kama hiyo ifikishwe bungeni ili tuijadili kuliko kuwaachia tu watalaamu .”
Kwa upande wake wakili na mwanaharakati wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kuwa makosa yalikwishafanyika tangu mwanzo hivyo, Serikali iwawajibishe walioingia mkataba huo au hata kushauri.

“Makosa yalishafanyika tangu mwanzo, hivyo Serikali iwajibike. Kinachoniuma mimi ni kodi za wananchi kutumika kulipia deni hilo. Wanaotakiwa kulipa hapo ni wale waliosaini mkataba huo au hata kushauri, ” alisema Sungusia.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alipotafutwa kwa njia ya simu alikuwa mkali na hakutaka kuzungumzia suala hilo.
“Wewe unataka mimi niseme nini? Kwanza uwe na adabu siyo kuuliza tu maswali. ‘I am not your age mate and I am not responsible to you…. Halafu unasema ‘what is my take… I don’t know,” alisema na kukata simu.
Licha ya maombi ya Tanesco, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliosomwa Alhamisi wiki hii na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elizabeth Mkwizu, ilitupilia mbali maombi hayo ya Tanesco na kuiamuru ilipe gharama za shauri hilo.
Katika uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walikubaliana na hoja za pingamizi la Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama, kuwa maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda.
Wakili Fungamtama katika hoja zake za pingamizi alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa nje ya muda kisheria. Alidai kuwa kisheria maombi hayo yalipaswa yawasilishwe katika muda wa siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu, lakini badala yake Tanesco iliwasilisha maombi hayo baada ya siku 351.
Akizungumzia uamuzi huo, wakili Fungamtama alisema kuwa sasa Mahakama ya Rufani imefungua milango kwa Dowans kukazia hukumu ya Mahakama Kuu ili iweze kulipwa fidia kama ilivyoamuriwa awali.
Hii ni mara ya pili kwa Tanesco kushindwa kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya Mahakama Kuu. Mara ya kwanza ilikuwa ni Septemba 6, 2012, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali maombi hayo.
Septemba 28, 2011, Mahakama Kuu iliiamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Sh94 bilioni na riba ya asilimia 7.5, hadi malipo ya mwisho yatakapokamilika, kufuatia tuzo iliyotolewa kwa Dowans na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).
ICC, katika hukumu yake ya Novemba 15, 2010, iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Dola za Marekani 65,812,630.03, kutokana na kuvunja mkataba wa kibiashara baina yake kinyume cha sheria.
Kufuatia uamuzi huo wa ICC, Dowans kupitia kwa wakili wake Fungamtama iliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya kusajili tuzo yake iliyotolewa na ICC, ili utekelezwaji wa malipo hayo uweze kuwa na nguvu ya kisheria.


MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.