SPIKA AHAIRISHA KIKAO CHA BUNGE BAADA YA WABUNGE KUTAKA MAJIBU KUTOKA KWA WAZIRI MKUU

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Hatimaye spika wa bunge Anna Makinda amelazimika kusitisha shughuli za bunge leo asubuhi baada ya wabunge kuchachamaa kumtaka waziri mkuu atoe majibu kuhusu tarehe ya kupiga kura ya maoni ya katiba kusogezwa mbele.
       Kizaazaa hicho kiliibuka baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) kuomba mwongozo wa Spika akitaka Bunge lisitishe shughuli zake na kujadili suala hilo la dharura kwa sababu hadi sasa hakuna mkoa uliomaliza kuandikisha wapigakura na hivyo kuleta utata kuhusu kura ya maoni ya katiba pendekezwa iliyopangwa kufanyika 30 Aprili mwaka huu.
            Baada ya Mnyika kutoa hoja hiyo huku akizomewa na wabunge wengi wa CCM, Spika Makinda alisema kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa kwa sababu linafanana na lile la kuifanyia marekebisho katiba ya sasa lililokuwa limehojiwa na mbunge mwingine, kwamba yote kwa pamoja yangetolewa majibu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo jioni wakati wa hotuba yake ya kuhairisha Bunge.
           Hata hivyo, uamuzi wake haukukubaliwa na wabunge hao wa upinzani ambao kwa pamoja walisimama na kuanza kupiga kelele wakisema “tunataka majibu…majibu kwanza mengine baadaye…Waziri Mkuu yupo pale atoe majibu”.
              Kelele hizo ziliendelea kwa takribani dakika saba na licha ya Spika kulazimisha Katibu wa Bunge kusoma ratiba ya utaratibu unaofuata, bado hakufanikiwa na hivyo kutangaza kuliahirisha Bunge kwa muda ahadi hapo baadaye.

No comments

Powered by Blogger.