POLISI WANASWA NA MENO YA TEMBO YAPATAYO 70 SAWA NA TEMBO 35


WATU tisa wakiwamo askari polisi wawili wa Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam wametiwa mbaroni wakiwa na meno 70 ya tembo (sawa na tembo 35).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, watuhumiwa hao walikamatwa Julai 28, mwaka huu usiku saa nne katika kizuizi cha Kauzeni, Kata ya Vikumbulu, wilayani Kisarawe wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 357 ABK aina ya Toyota Surf.
Aliwataja askari hao kuwa ni Senga Idd Nyembo na Issa Mtama.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na askari hao ni Hamidu Hamadi na Prosper Maleto wakazi wa Tandika, jijini Dar es Salaam, Mussa Mohamed Ali mkazi wa Kinondoni, Amir Bakari mkazi wa Mbagala, Seif Kadro Mdumuka mkazi wa Kisarawe, Said Kadro Mdumuka na Ramadhani Athuman wakazi wa Chanika.
Kamanda Matei alifafanua kuwa meno hayo yana uzito wa kilo 305, yakiwa na thamani ya sh 850,500,000, huku akitoa wito kwa wananchi kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili ili wachukuliwe hatua bila kujali nyadhifa zao.
Katika hatua nyingine, mkazi wa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, Ibrahim Mnyanga (58) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na vipande 16 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 24.5 kinyume cha sheria.
Mnyanga alikamatwa Julai 22, mwaka huu, saa tisa alasiri eneo la Msimbazi Centre akiwa na masanduku mawili yenye nyara hizo za serikali.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na askari polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliokuwa kwenye doria ya kawaida kumtilia shaka.

Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema kuwa atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Kova aliongeza kuwa ameunda jopo la uchunguzi wa kifo cha mtuhumiwa Seleman Mwinyi (46) mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, jopo la uchunguzi linaundwa na Jeshi la Polisi, vyombo vya ulinzi na usalama wakishirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).
Marehemu Mwinyi alikutwa na mauti akiwa ndani ya chumba cha mahabusu Kituo cha Polisi Oysterbay huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni akidai kwamba kifo cha mtuhumiwa huyo kilitokana na kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira.


TANZANIA DAIMA

No comments

Powered by Blogger.