MTANZANIA ADAKWA NA HEROINE MAREKANI

  Abainika kuzificha kwenye `laptop`
  Kutupwa jela miaka 40
Balaa lingine limeikumba nchi baada ya Mtanzania Joseph Makubi (33), kukamatwa nchini Marekani, akiwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya Heroine alizozihifahi kwenye kompyuta ndogo maarufu kama laptop.
Makubi ambaye amepandishwa kizimbani kujibu mashtaka, aliweka dawa hizo kwenye laptop mbovu, iliyokamatwa muda mfupi baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Los Angeles, akitokea Nairobi nchini Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Habari la The Associated Press (AP) na San Jose Mercury News-California (yote ya Marekani) zilizochapishwa kwenye mtandao, Makubi alikutwa na heroine yenye uzito wa gramu 800.
AP ilikariri taarifa za shirika la habari la City News Service, likiandika kuwa Makubi, aliyefikishwa katika Mahakama ya Jimbo la Los Angeles, Jumatano wiki hii, alikiri kosa la kufanya biashara hiyo nchini Marekani.
Kufuatia kukiri huko, Makubi anatarajiwa kupewa hukumu ya kifungo cha miaka 40 jela na sasa yuko rumande akisubiri kuanza kifungo chake Septemba Mosi mwaka huu, kwa mujibu wa sheria za Marekani.

AP ilikariri taarifa za Mkaguzi wa Idara ya Forodha ya uwanja wa ndege wa Los Angeles, zikieleza kuwa laptop ya Makubi ilikuwa nzito `kupindukia wakati ilipopekuliwa.
“Tulijaribu kuiwasha lakini haikuwaka na kubaini kuwa ilikuwa imeharibika, tulipofunguliwa tulibaini kuna gramu 800 za heroine,” mtandao huo ulikariri chanzo cha taarifa hiyo.
Makubi aliwaambia maofisa wa uwanja huo kuwa alitoka Nairobi, Kenya na alikwenda Los Angeles akiwa njiani kuelekea Alabama kukutana na mwanamke aliyekuwa anawasiliana naye kupitia mtandao wa ‘internet’.

 Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini

Matukio ya Watanzania kukamatwa na dawa za kulevya yanatisha kutokana na wengi kunaswa na mihadarati sehemu nyingi duniani ikiwamo China, Pakistan, Hong Kong , Kenya na Afrika Kusini.
Pia Tanzania inatajwa kuwa na idadi kubwa ya wafungwa kwenye magereza ya ughaibuni, waliopatikana na hatia za kusafirisha dawa hizo kwa kubeba tumboni au kuzisafirisha kwa kutumia mbinu nyingine.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, sasa unaelezwa kuwa ni kitovu cha kupitisha dawa hizo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments

Powered by Blogger.