ENEO LA AJALI YA SUMRY SINGIDA LIMESHAUA 50

 Majeneza yenye miili ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliofariki dunia baada ya kugongwa na basi wakati wakipima ajali  katika kijiji cha Utaho wilani Ikungi mkoa wa Singida kabala ya kuagwa na kusafirishwa kwenda makwao. Picha na Gasper Andrew 
Wakati miili 15 ya marehemu waliofariki dunia kwa kugongwa na basi katika Kijiji cha Utaho mkoani Singida ikizikwa juzi, imeelezwa kuwa eneo hilo limekithiri kwa ajali hadi kuwatisha wanakijiji.
Wakazi wa kijiji hicho walisema jana kuwa ndani ya miaka minne, zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha katika eneo hilo kutokana na ajali kiasi cha kuingiza hisia za imani za kishirikina.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Selemani Kinanda alisema: “Kwa miaka minne iliyopita, ukiacha marehemu 15 wa juzi, watu karibu 50 wamepoteza maisha. Wengi ni vijana wa kiume.”
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Alisema naye aliwahi kupata mikasa katika eneo hilo na kujikuta amejibamiza kwenye gari na kuhama barabarani hadi kichakani na baiskeli yake, baada ya kuona ‘mauzauza’ kwenye eneo hilo.
“Kwanza yule aliyegongwa kwanza na kusababisha yote haya hatujui alitokea wapi, pia kulikuwa na sababu gani kwa dereva huyu wa basi kuwafuata watu hao wote pembeni na kuacha barabara kubwa kulia kwake? Hatukusikia gari ni bovu wala tairi limepasuka, lazima kuna mkono wa mtu,” alisema Fatuma Shabani, aliyefiwa na kaka yake.
Hata hivyo, taarifa kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani zinasema kuwa hakuna takwimu zozote zinazoonyesha idadi ya ajali au vifo katika eneo hilo, zaidi ya ile ya juzi yenye takwimu sahihi.
Majonzi kijijini
Kijiji kizima cha Utaho tangu juzi kilikuwa katika majonzi na simanzi, hata baada ya miili ya marehemu wanane wa ukoo mmoja na wengine saba wahamiaji kutoka vitongoji vya Maguha na Kinyaghaa kuzikwa katika makaburi ya kimila kijijini hapo.
Kutokana na familia nyingi kuwa na msiba, watu walionekana wakitoka nyumba moja kwenda nyingine kutoa pole.
“Msiba ulikuwa mgumu, tulikuwa tukichimba kaburi hapa tunazika, tunakwenda kwa mwingine. Kilio hiki ni cha ajabu na miujiza sana kwetu,” alisema Ramadhani Nyange (74) na kuongeza: “Tunashindwa tuanzie wapi au kwa nani, maana sisi wote ni ndugu, tumeoleana na kuzaliana kutoka kwa babu yetu Bulali Masuja ambaye ni mwanzilishi wa kijiji tangu mwaka 1972.”
Alisema kuna haja ya kufanya mkutano wa ukoo ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Watu hao ni miongoni mwa 19 waliokufa katika ajali hiyo wakiwamo mwenyekiti wa kijiji, ofisa mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji pamoja na askari polisi wanne. Watu wengine wanane walijeruhiwa.
Aidha, wananchi hao walionyesha wasiwasi juu ya shughuli za maendeleo baada ya kufiwa na viongozi wote na juu ya Sh10 milioni za kijiji zilizoko benki.
Mazishi ya polisi
Mazishi ya askari F 6837 PC Jumanne Mwakihaba yalifanyika jana saa 7:00 mchana katika makaburi ya Kisarawe Mjini, yakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kisarawe (OCD), Issa Lutavi.
Mwili wa marehemu ulifikishwa nyumbani kwao Kisarawe alfajiri jana na ulizikwa kwa taratibu za kijeshi. Mwakihaba alijiunga na jeshi hilo Agosti 30, 2004 na kupangiwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Singida ambako mauti yamemkuta.
Habari zilizopatikana mkoani Kilimanjaro, zilisema kuwa mwili wa G. 7993 Novatus Tarimo utazikwa kesho huko Tarakea, Rombo.
Kikwete atuma salamu
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Perseko Kone kutokana na ajali hiyo iliyosababisha vifo hivyo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema jana kuwa Rais amesikitishwa na ajali hiyo iliyopoteza nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa Taifa.
“Vifo hivi hakika vimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu,” taarifa hiyo ilimkariri Rais Kikwete.
Pamoja na kuwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo, Rais Kikwete aliwaombea kwa Mungu watu wote waliojeruhiwa wapate kurejea haraka katika hali zao za kawaida.
 MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.